SwahiliHub on Sept 1, 2015

WASHINDI WA INSHA ZA KIDIJITALI KUTUNUKIWA VIPAKATALISHI

Will receiving devices

Meneja wa Mauzo Taifa Leo na Swahili Hub Bw Brian Mwake (kati) ashuhudia Bw Hezekiel Gikambi (kulia) akimkabidhi Bw Will Clurman vipakatalishi sita aina ya ASUS katika jumba la Nation Septemba 1, 2015. Picha/ANTHONY OMUYA

Na HEZEKIEL GIKAMBI

Imepakiwa – Tuesday, September 1  2015 at  17:18

Kwa Mukhtasari

Mkumbo wa tatu wa mashindano ya insha za kidijitali unaoandaliwa na kampuni ya E-kitabu na kushirikisha kaunti zote nchini Kenya umekamilika wiki hii kwa kupatikana kwa washindi 12 huku zawadi zao zikiandaliwa.

 

MKUMBO wa tatu wa mashindano ya insha za kidijitali unaoandaliwa na kampuni ya E-kitabu na kushirikisha kaunti zote nchini Kenya umekamilika wiki hii kwa kupatikana kwa washindi 12 huku zawadi zao zikiandaliwa.

Washindi hawa watatu kutoka shule za upili na watatu kutoka shule za msingi katika vitengo viwili cha Kiswahili na Kiingereza watatunukiwa zawadi mbali mbali zikiwa ni pamoja na vipakatalishi, karo ya shule, vifaa vya kielekroniki vya kisomea vitabu kama ‘tabuleti’, vyeti na kadhalika.

Kati ya wadau wakuu wa shindano hili ni kampuni ya Nation Media kupitia kwa gazeti la Taifa Leo na tovuti ya Swahilihub ambayo inafadhilia zawadi za vipakatalishi sita kwa ajili ya kutunukiwa kitengo cha Kiswahili, katika shule ya msingi na shule ya upili wanafunzi watatu bora kwa kila kiwango.

Hafla ya kutoa zawadi itafanyika mnamo tarehe 23 Septemba, 2015 katika Maonyesho ya 18 ya Kimataifa ya Vitabu ya Nairobi katika ukumbi wa Sarit Centre.

Akizungumza katika jumba la Nation Centre Jumanne, wakati wa kupokea zawadi hizo, Afisa Mkuu mtendaji wa e-Kitabu Bw Will Clurman alishukuru kampuni ya Nation Media kwa ishara hiyo ya kuunga mkono jukwaa la kidijitali na kufadhilia mashindano hayo ya insha.

“Nation kupitia Swahilihub wameonyesha kuwa jukwaa la kidijitali ni uhalisia wa maisha katika karne hii hapa nchini Kenya hata kwa lugha ya kiasili kama Kiswahili. Tunawashukuru kwa kuwatuza washindi wa Kiswahili vipakatalishi hivi,” akasema Bw Clurman.

Maandalizi ya siku ya tuzo

Hafla hiyo iliwashirikisha Bw Hezekiel Gikambi anayesimamia tovuti ya Swahilihub na Bw Brian Mwake ambaye ni Meneja wa Mauzo wa gazeti la Taifa Leo na Swahilihub waliomkabidhi Bw Clurman vifaa hivyo ili afanye maandalizi ya siku ya kutuzwa baadaye Septemba.

Hafla ya kuwatunuku zawadi wanafunzi washindi inatarajiwa kuhudhuriwa na Waziri wa Mawasiliano Bw Fred Matiang’i.

E-kitabu ni jukwaa la kwanza nchini Kenya kuuza vitabu vya kidijitali wakishirikiana na matbaa mbali mbali na Wizara ya Elimu.

Wafadhili wengine ni kama kampuni za kompyuta za HP, Mustek, Toshiba, na kadhalika.

hgikambi@ke.nationmedia.com

Original article:  http://www.swahilihub.com/habari/MAKALA/washindi-wa-Insha-za-kutunukiwa-vipakatalishi-/-/1310220/2854530/-/126303sz/-/index.html