Eileen Chepng’eno – Kericho Primary School

Kwa  Mpendwa  Rais ,

Maisha yangu kama mwanafunzi wa kidijitali  yamekuwa  ya kushusha moyo. Mimi ni mwanafunzi  mwenye idili za mchwa kichuguuni. Nina nia kuu na azma ya kuwa mtu mashuhuri hapo mbeleni. Sitakubali hata kamwe kitu chochote kinizuie kupata azimio langu.

Mara tu niliposikia habari kuhusu vipakatalishi kwenye redio nilifurahi. Nilifurahi kuzidi mvuvi  mkata asiye na be wala te na alikinasa kishazi  cha samaki. Kweli nilikuwa na sababu ya kufurahi kuzidi ghaya. Nilikula yamini kuwa  lazima kama ibada wavyele wangu wangekupigia kura, pindi tu waliposikia habari hizi walifurahi upeo wa kufurahi. Wazazi wangu walionelea kuwa ungeingia ofisini muda wa bana banua.

Hivi majuzi walimu wetu walienda katika mkutano wa shule za serikali. Nilisikia walienda kuzungumza kuhusu vipakatalishi hivi. Nilijawa na furaha kwani baada ya mkutano vipakatalishi hivi vingeletwa. Nilijipa shime kuwa vipakatalishi hivyo hatimaye vilikuwa vimefika

Vipakatalishi hivi vina faida tumbi nzima.Masomo yatakuwa rahisi mofimu hizi za kidijitali zitumiwapo. Wanafunzi wataweza kuelewa vitu kwa urahisi  na pia  zitashusha gharama ya kununua vitabu vya kusoma. Wanafunzi wataweza kupata vitabu chungu nzima katika vipakatalishi hivi. Vitabu hivi vitawafaidi kwa hali na mali. Wavyele hawatajawa na shida za kununua vitabu.

Mwalimu anaweza kupiga picha ya kitu kama vile mlima. Mwalimu huyu akitaka kufunza kuhusu mlima huo ataleta picha hiyo na kuweka kwenye projekta. Kutokana na hii, masomo yataendelea bila kudhuru mazingira. Wanafunzi wataweza kuelewa vitu kwa urahisi.

Picha hizi hutumiwa kueleza zaidi kuhusu jambo ambalo wanafunzi hawakulijua.Hii itawafanya wanafunzi wajadiliane kuhusu mambo ambayo bado hayajaeleweka.

Mwalimu anaweza kutuma kazi ya ziada kwa wanafunzi hata  akiwa safarini. Hii itawafanya hasa wale wa darasa la nane kuerevuka zaidi. Maadam wafanyapo kazi hii hujikumbusha mengi. Walimu wetu marakwa mara wamepiga kelele kuhusu kifutio chetu. Husema hakifuti vizuri.Vipakatalishi hivi vinaweza kuwanyamazisha.Isitoshe, vitabadilisha kutumia madaftari   kufanya kazi ya ziada, hivyo hushusha gharama ya kununua.

Wavyele wangu wamekuwa wakishangaa na kubung’aa.Wameshinda   wakiuliza ni lini vipakatalishi hivi vitawasili. Imekuwa ni muda wa paka kunawia mate tangu utuahidi. Wahenga na wahenguzi hawakutupwayapwaya kwa mipwayo walipodhukuru kisha kunadi, ahadi ni deni.Katika familia yangu ni mimi pekee nimeelimishwa kwani wavyele wangu ni fukara hohehahe. Wazazi wangu ni walalahoi wasio na be wala te. Mimi ndiye nitaonyesha mfano mwema kwa wadogo wangu.

Ni masikitiko makubwa kuwa vipakatalishi hivi vitakuwa vya wanafunzi wa darasa la kwanza tu. Rais, ingekuwa bora zaidi kama ungeanzia madarasa ya cheo cha juu.  Tutaweza kuelewa zaidi nakusawazishwa na wanafunzi wa shule za kibinafsi. Nitajawa na furaha ukianzia madarasa ya cheo cha juu.

Ukianza madarasa ya cheo cha juu itakuwa itakuwa jambo aula. Hii itashusha kwa njia kubwa pana   ambalo limo kati ya shule za kibinafsi na za serikali. Watoto wa shule za serikali na za kibinafsi wataweza kushindana bila tatizo lolote.

Hivi majuzi niliposikia kuhusu habari zile za Kilifi nilifurahi ghaya ya kufurahi. Wanafunzi wa Kilifi sasa hivi wanajua kuongea lugha nathari bila doa wala kasoro. Waliweza kujieleza katika redio. Inabainika bayana na imeshamiri    kote mithili ya moto nyikani kuwa Kilifi huvuta mkia lakini sasa naona mambo yakiwa mengine. Wanafunzi wa mwaka huu wamo teyari tahayuti kufanya mtihani huo. Vipakatalishi hivi vimewafaa sana.  Itakuwa jambo aula ukifanya hivi katika kaunti zote.

Nitazama katika lindi la furaha vipakatilishi hivi vikifika kwetu.Itakuwa vyema mambo haya yakifanywa chapuchapu.