Nyagaka Sandra Bonareri – Moi Girls, Eldoret

Kwa mpendwa Rais…Maisha yangu kama mwanafunzi wa kidijitali yameuchukua mkondo mpya tangu kuidhirishwa kwake, Kuwa mwanafunzi wa kidijitali siwezi kusema kuwa kumeifaidi mimi tu bali pia wanafunzi wengi nchini. Yakini, maisha yangu yameuchukua mkondo mpya, nayo yamenitia azma ya kutia bidii masomoni. Hii ni afueni kwangu na kwa wanafunzi wengine ambao wamo kwenye safari ya kuyajenga maisha yao.

Kugura kutoka kwa sekta ya kale ya kimasoma hadi kufikia umbali huu wa kidijitali kumekuwa na faida si haba. Aisee! Maisha yangu kama mwanafunzi wa kidijitali yametoka katika kiza na kuwekwa katika mwanga utakaoniwezesha kutimiza ndoto yangu ya kuwa mtu wa faida kwa jamii yangu katika siku za halafu. Baadhi ya mambo yanayochangia mimi kuwa mwanafunzi wa kidijitali ni walimu, shule yangu na mandhari ninamoishi.

Tangu mfumo wa dijitali kuingia katika ulingo wa masomo, makongamano ya sayansi yamekua kwa kiasi kikubwa. Kabla ya mfumo huu, makongamano haya yalikuwa adimu au niseme tu yalikuwa mithili ya wali wa daku. Wanafunzi walipojitosa katika uwanja wa dijitali kwa kutumia tarakilishi katika utafiti wao, wengi wao walifaidika na wanazidi kufaidika. Ingawa bado sijapata fursa ya kujiunga na makongamano haya, kuna mafunzo ninayopata kutoka kwa vipindi hivi ambavyo hunisaidia kukuza alama zangu katika masomo ya sayansi.

Kati ya matatizo yanayoniandama kama mwanafunzi wa kidijitali ni mtandao. Mtandao huu wakati mwingi hunifanya kuwa mvivu katika kufanya gange za darasani na za ziada. Ninapokuwa nyumbani, mara nyingi hujipata nimeviasi vitabu vyangu na kuitwaa simu ili kuingia mtandaoni kwa takriban siku nzima. Kinachoshangaza zaidi ni kuwa, hata ninapoonywa na wazazi wangu, hujipata nimenyapia simu na kuitumia huku nikiviziarizia nisipatikane. Tabia hii hupoteza muda mwingi wa masomo.

Tatizo jingine ni shinikizo la hirimu ambalo limeathiri si mimi tu bali wanafunzi tumbi nzima. Ningependa kujihimiza na kuwahimiza wanafunzi wote kuwa, tuna satua ya kujiokoa kutoka kwenye bahari hii haraka iwezekanavyo. Tusisubiri kuimbiwa wimbo wa kuyachuja maisha yetu kwani tumejaaliwa akili razini ya kujua kinachofaa na kisichofaa. Wenye lugha walisema, gogo la mbugu si la mvule.

Ningependa kutoa shukrani zangu chekwa kwako Rais wa Jamhuri ya Kenya, mheshimiwa Uhuru Kenyatta kwa kazi aula unayofanya na serikali yako. Siwezi katu kuuweka ukarimu wako kwenye mizani niupime uzito wake kwani haitowezekana. Juhudi unazozifanya kunisaidia kuyainua masomo yangu kutoka kiwango kimoja hadi kingine, nakuahidi ya kuwa hazitakuwa za bure bilashi. Ni tayari katika mwendo wa kukwangura alama murua ili kulisaidia taifa letu.

Kuwa mwanafunzi wa kidijitali ni fanaka kwangu. Wale wote ambao hawajapata fursa ya kusoma kidijitali, wasione hawafai kwani, kila likuepukalo mja, lina heri nawe!

Ningependa kusema kuwa vipindi vya televisheni na redioni vinavyopeperushwa hewani katika stesheni tofautitofauti nchini vimenisaidi si haba. Mfano aula ni kipindi kinacholetwa kila siku ya Jumamosi runingani, kiitwacho ‘kamusi ya Changamka’ katika kituo cha televisheni cha QTv, chenye watangazaji wakwasi wa lugha ikiwemo Wallah bin Wallah na Muneno Nyaga. Mfano mwingine ni kwenye rungoya katika stesheni ya Radio Citizen kiitwacho ‘Bahari ya Lugha,’ chenye watangazaji mahiri kama vile Hassan Mwana wa Ali. Vipindi hivi haviburudishi tu bali pia vinanisaidia kuikuza lugha ya Kiswahili.

Tangu kuwepo kwa matumbuizo kutoka kwenye video, muziki na sanaa za maonyesho yanayolenga kuwafundisha wanafunzi elimu ya vitabuni na ya maisha, imenisaidia kwa kiwango kikubwa. Waigizaji wanapoigiza ukumbini, maonyesho haya huwa na mnato akilini yanayonisaidia kukumbuka mtiririko wa hadithi na riwaya. Maonyesho haya pia hunisaidia kuyajibu maswali katika riwaya tunazotahiniwa katika mitihani.

Waliamba weledi wa lugha kuwa, kizuri hakikosi ila. Nami basi singeweza kukwepa kutaja walakini wa kuwa wanafunzi wa kidijitali. Afueni iliyoko ni kuwa, ila hizi si nyingi zikilinganishwa na faida zinazotokana na mfumo wa masomo ya kidijitali. Niseme tu ni kiasi cha kuweza kugandamizwa na walimu na wanafunzi wote nikiwemo mmoja wao. Ninachamini ni kuwa nikijitolea mhanga kujiepusha na kasoro hizi, mwishowe nitafaulu.